Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, aliyasema hayo katika hafla ya kumuenzi Mkurugenzi wa zamani na kumtambulisha Mkurugenzi mpya wa Hawza ya eneo la Kashan Iran. Hafla hiyo ilifanyika mchana wa leo katika Msikiti Mkuu wa Swala ya Ijumaa wa mji huo, ikihudhuriwa na wanazuoni, walimu, wanafunzi wa Hawza pamoja na baadhi ya viongozi na watu mashuhuri katika nyanja za kielimu na kiutamaduni.
Katika hafla hiyo, Ayatullah Arafi alizishukuru juhudi za wakurugenzi waliotangulia, huku akimpongeza Mkurugenzi mpya na kumtakia mafanikio. Pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha nafasi ya kielimu, kiutamaduni na kijamii ya Hawza ya Kashan.
Mwanzoni mwa hotuba yake, baada ya kumhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, alisema: “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia tena fursa ya kufika katika eneo hili lenye historia ya fahari, lililo mstari wa mbele, lenye historia ndefu, lililochangia kujenga utamaduni na lenye historia kubwa ya Hawza. Mwanzoni mwa hotuba yangu, tunatoa salamu zetu kwa Mitume wa Mwenyezi Mungu, Mawalii wa Mwenyezi Mungu, Imam Khomeini (r.a), Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Mashahidi wote wenye daraja tukufu, hususan mashahidi wa eneo hili. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie sote tawfiki ya kuifuata njia ya mashahidi.”
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akiwashukuru wanazuoni, viongozi wa dini, walimu, wanafunzi wa Hawza, viongozi wa serikali, wakurugenzi na wananchi wa heshima wa Kashan waliohudhuria hafla hiyo, aliongeza: “Nawashukuru kwa dhati watu wote waheshimiwa walioshiriki katika mkusanyiko huu wa kielimu na kiroho. Hata hivyo, tunapaswa kuzingatia kwamba chanzo na asili ya shukrani zote ni Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu kila mafanikio na huduma hatimaye hutokana na fadhila na neema za Mwenyezi Mungu.”
Akizungumzia historia ya kidini, kielimu na kiutamaduni ya wananchi wa eneo la Kashan, alibainisha kuwa wananchi wa eneo hilo katika kipindi chote cha historia wamekuwa pamoja na elimu, fikra, dini, fasihi na maadili, na wamekuwa na mchango mkubwa katika kuiunga mkono Hawza na kueneza mafundisho ya dini.
Ayatullah Arafi pia akizungumzia ushiriki na nafasi ya wananchi katika matukio na vita vya hivi karibuni, alisema: “Wananchi wa heshima wa eneo hili, kama ilivyo kwa taifa kubwa la Iran, wamekuwa na ushiriki wenye ufanisi na wa kuamua katika nyakati nyeti na zenye kuamua hatima ya nchi. Ushiriki wa wananchi sambamba na vikosi vya ulinzi na usalama, pamoja na kuunga mkono uongozi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ulikuwa ni kielelezo cha wazi cha uelewa wa kisiasa na kidini, kuwa mstari wa mbele na uaminifu wa taifa la Iran kwa dini, Mapinduzi na tunu za Kiislamu.
“Enyi wananchi waumini na wenye heshima, siku zote mmekuwa mstari wa mbele katika kulinda dini, maadili na tunu za Mwenyezi Mungu. Hii ni tunu kubwa ya kijamii na kidini inayostahili kuthaminiwa.”
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran aliendelea kwa kuwashukuru viongozi wa dini, wanafunzi wa kike na wa kiume wa Hawza, walimu, wakurugenzi na viongozi wa eneo hilo. Pia alizishukuru juhudi za mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Kashan, pamoja na watu wengine mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo.
Alisema: “Waheshimiwa wote waliojitahidi katika njia ya maendeleo ya kielimu, kiutamaduni na ya Hawza katika eneo hili wana mchango katika kufanikisha harakati hii yenye thamani.”
Vilevile, alizikumbuka na kuenzi kumbukumbu za wanazuoni waliofariki dunia na watu mashuhuri katika historia ya Hawza, akiwemo Ayatullah al-Udhma Khurasani na Ayatullah al-Udhma Shubairi Zanjani, huku akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi urithi wa kielimu na kiroho wa watu hao wakubwa.
Basij ni miongoni mwa rasilimali kubwa za Mapinduzi ya Kiislamu
Ayatullah Arafi, akizungumzia kuwadia kwa Wiki ya Basij, alisema: “Basij ni miongoni mwa rasilimali kubwa za Mapinduzi ya Kiislamu, ambazo zimefungamana na fikra za juu za Imam Khomeini (r.a), na katika miaka iliyopita zimekuwa chanzo cha baraka nyingi kwa nchi. Tunatumai kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaweka mashahidi wote na wapiganaji waliojitolea katika njia hii miongoni mwa waja Wake wema na waliokaribu Naye.”
Aidha, akiupongeza umma wa Kiislamu kuwadia kwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa furaha kwa Bibi Fatimah Zahra (amani iwe juu yake), pamoja na kuadhimishwa Siku ya Mwanamke, alieleza nafasi ya juu ya Bibi huyo katika mfumo wa maarifa ya Uislamu.
Khutba ya Fadak: Katiba ya Mwenyezi Mungu ya kutambua neema na wajibu wa mwanadamu
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizungumzia khutba ya kihistoria ya Bibi Fatimah Zahra (s.a) katika Msikiti wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), alisema: “Mwanzoni mwa sehemu hii ya hotuba yangu, naona inafaa kukumbusha sehemu ya Khutba ya Fadak ya Bibi Zahra (s.a), ambayo Bibi huyo mtukufu aliitoa katika Msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, mbele ya watu waliokuwepo. Kupitia maarifa yake ya juu ya Mwenyezi Mungu na hotuba yake yenye msisimko na msimamo thabiti, hakuwahutubia tu watu waliokuwepo msikitini, bali pia aliielekeza hotuba yake kwa dhamiri ya historia na ya mwanadamu kwa ujumla.”
Aliongeza kuwa baada ya mazingira ya msikiti kubadilika kutokana na uwepo na hotuba ya kihistoria ya Bibi Fatimah Zahra (s.a), alianza hotuba yake kwa kumhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Khutba ya Fadak, kwa kuzingatia maudhui yake, muundo wake, fasihi yake na maarifa yake ya juu ya Mwenyezi Mungu, ni miongoni mwa mifano bora zaidi ya utoaji wa hotuba katika Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s). Tangu mwanzo wake, khutba hiyo imekuwa ikipewa umuhimu katika vyanzo na urithi wa kielimu wa Mashia na Ahlu Sunna.
Ayatullah Arafi, akizungumzia sehemu za mwanzo za Khutba ya Fadak na kueleza mtazamo wa Bibi Fatimah Zahra (s.a) kuhusu neema za Mwenyezi Mungu, alisema: “Katika sehemu hii fupi tu ya khutba, kuna ulimwengu mzima wa ukweli wa kimaarifa na wa mbinguni unaohusu neema za Mwenyezi Mungu.”
Akieleza kwamba neema za Mwenyezi Mungu zina sifa muhimu na za msingi, alisema: Jambo la kwanza ni kwamba neema zote za Mwenyezi Mungu zimeenea katika ulimwengu mzima wa uwepo na katika maisha ya mwanadamu. Hakuna kiumbe chochote kinachoweza kujitosheleza bila neema na fadhila za Mwenyezi Mungu.
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran aliendelea kusema kuwa sifa ya pili ya neema za Mwenyezi Mungu ni kwamba neema hizo hazina chanzo cha awali kutoka kwa mwanadamu mwenyewe. Yaani, kabla ya mwanadamu kuzipata neema hizo, hakuwa na chochote alichokuwa nacho ambacho kingempa haki ya kudai kuwa anastahili kupewa neema hizo na Mwenyezi Mungu.
Asili ya uwepo wa mwanadamu, uhai wake, vipaji vyake na uwezo pamoja na rasilimali alizonazo, vyote vinatokana na fadhila na neema za Mwenyezi Mungu.
Alitaja sifa ya tatu ya neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni mwendelezo na mnyororo wa neema, akisema: “Neema za Mwenyezi Mungu hazijatengana moja na nyingine, bali zinatolewa kwa mwanadamu na ulimwengu mzima wa viumbe katika mfumo mmoja ulioungana na wenye mshikamano. Kila neema inaendelea kutokana na neema nyingine, na kwa pamoja zinaunda mkusanyiko mkubwa usio na mwisho.”
Ayatullah Arafi, akizungumzia kutoweza kwa mwanadamu kulipa fadhila za neema za Mwenyezi Mungu, alibainisha: “Mwanadamu anapojikuta mbele ya mfumo mkubwa kiasi hiki wa neema, inakuwa wazi kwamba hana uwezo wa kuzihesabu zote kikamilifu, wala hawezi kutekeleza kikamilifu haki ya kuzishukuru.
“Leo, katika falsafa na mwelekeo wa Mapinduzi ya Kiislamu, tunasisitiza kuwasilisha mfano tofauti na ulio bora zaidi wa maisha ya mwanamke muumini na Muislamu. Mfano ambao mizizi yake inatokana na mwenendo na haiba ya Bibi Fatimah Zahra (s.a).”
Aliongeza: “Bibi Zahra (s.a), licha ya kufikia kilele cha kujisitiri, hali ya kiroho, ibada na maarifa ya Mwenyezi Mungu, pia alishiriki kwa uwajibikaji katika kushughulikia masuala ya msingi ya jamii. Kupitia hotuba zake za kina, zenye hoja na msimamo thabiti, alijitokeza kwa ajili ya kuiongoza na kuiokoa jamii ya mwanadamu.”
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, alibainisha kuwa mwanamke huyo mtukufu ni mfano kamili kwa mwanamke Muislamu; mfano unaojumuisha hali ya kiroho, elimu, maarifa, uwajibikaji wa kijamii, kutetea haki na kushiriki kwa uelewa katika matukio yanayoamua hatima ya jamii.
Akisisitiza umuhimu wa kuutambulisha mfano huo duniani, alisema: “Moja ya majukumu yetu muhimu ni kuutambulisha kwa jamii ya kimataifa mfano wa maisha ya mwanamke Muislamu na nafasi ya maisha ya kijamii ya mwanamke katika fikra za Kiislamu. Huu ni ukweli unaopaswa kuelezwa kwa wanadamu wote kwa kutumia lugha ya mantiki, maarifa, hoja na mwenendo wa vitendo wa Ahlul-Bayt (a.s).”
Ayatullah Arafi, akizungumzia jinsi kambi ya ubeberu inavyokuwa makini na yenye wasiwasi kuhusu kuenea kwa ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: “Maadui wanafahamu vizuri kwamba iwapo maarifa na ujumbe huu wa Mwenyezi Mungu utaenezwa duniani kwa usahihi, utazalisha uwezo mkubwa wa kuamsha uelewa, harakati na mabadiliko katika jamii za wanadamu. Kwa sababu hiyo, wanapambana na kuenea kwa ujumbe huu.”
Hawza na umuhimu wa kulinda jukumu la kijamii na kisiasa la viongozi wa dini
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, katika sehemu nyingine ya hotuba yake, akizungumzia ujumbe wa kihistoria wa Imam Khomeini (r.a) kuhusu majukumu ya Hawza na viongozi wa dini, alisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kushiriki kwa uelewa katika nyanja za kijamii na kisiasa.
Akizungumzia hoja zilizojadiliwa katika ujumbe wa Imam Khomeini kuhusu shahada na nafasi ya mashahidi, alisema: “Imam Khomeini (r.a), katika jumbe zake, hususan jumbe zinazohusiana na shahada na njia ya mashahidi, alisisitiza wajibu wa kihistoria wa viongozi wa dini na Hawza katika kuulinda Uislamu, kuitetea nchi na kukabiliana na mikondo potofu.”
Ayatullah Arafi aliendelea kusema: “Moja ya madhara ambayo Imam Khomeini (r.a) alikuwa akionya mara kwa mara ni mkondo wa kujifanya mtakatifu; mkondo ambao ulijitahidi kuitenga Hawza na masuala ya msingi ya jamii, na kwa kuuwekea mipaka wajibu wa kijamii na kisiasa wa viongozi wa dini, kuandaa mazingira ya kueneza fikra za kuitenganisha dini na siasa.”
Alifafanua kuwa mkondo huo hatari unaonyesha kuwa ushiriki wa Hawza katika masuala muhimu ya wananchi, mabadiliko ya kijamii na kisiasa, pamoja na mapambano dhidi ya dhuluma na ufisadi, si jambo sahihi. Badala yake, unawahimiza viongozi wa dini kukaa kimya, kujitenga na jamii na kujiepusha na masuala ya kisiasa.
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran alibainisha: “Hali ni kwamba viongozi wa dini wa kweli na Hawza katika kipindi chote cha historia wamekuwa pamoja na wananchi, wakishiriki katika medani za kutetea dini, uadilifu na tunu za Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, haiwezekani kupunguza jukumu la Hawza na kulifungia katika shughuli finyu za ufundishaji na masuala ya mtu binafsi pekee.”
Historia ya Kashan: Kutoka kuupokea Uislamu kwa uelewa hadi kuwalea wanazuoni wakubwa
Ayatullah Arafi, akiendelea na hotuba yake na kuzungumzia historia ya Kashan pamoja na urithi wake wa kielimu, alisema kuwa uwezo wa eneo hili unavuka mipaka ya Hawza ya eneo husika alisema: “Ili kuitambua nafasi ya Hawza ya Kashan, tunapaswa kurejea katika kurasa zenye fahari za historia ya eneo hili; kurasa zinazoonyesha kina cha utamaduni, dini na elimu ya wananchi wa ardhi hii.”
Aliongeza kuwa moja ya sifa muhimu katika historia ya Kashan ni jinsi wananchi wa eneo hilo walivyoupokea Uislamu na maarifa ya kidini mapema na kwa mapenzi makubwa. Mapokezi hayo hayakuwa ya juu juu wala ya kuiga tu, bali yaliambatana na utambuzi, uelewa na misingi ya kiutamaduni na kifikra.
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia historia ya Ushia katika eneo la Kashan, alisema: “Wananchi wa eneo hili waliupokea kwa mapenzi na uelewa mwenendo na mafundisho ya Ahlul-Bayt (a.s). Katika kipindi chote cha historia, hatua kwa hatua walivuka nafasi ya kuwa wapokeaji wa maarifa ya kidini na kuwa washiriki pamoja na wazalishaji wa elimu na utamaduni wa Ahlul-Bayt (a.s).
“Katika eneo hili wamekuwepo daima wanazuoni na watu mashuhuri ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kueneza maarifa ya Ahlul-Bayt (a.s), kuendeleza elimu za Kiislamu na kuimarisha misingi ya maarifa katika jamii.”
Ayatullah Arafi, akisisitiza umuhimu wa kizazi kipya kuifahamu historia hiyo, alisema: “Wanafunzi wa shule, wanafunzi wa vyuo vikuu, wanafunzi wa Hawza na vijana wa Kashan wanapaswa kufahamu kurasa zenye fahari za historia na utambulisho wa kielimu na kidini wa eneo lao. Kuufahamu urithi huu wenye thamani kutaimarisha utambulisho wa kiutamaduni na kidini wa kizazi kipya, na kuweka mazingira ya kujisikia kuwajibika zaidi kuhusu mustakabali wao.”
Hawza ya Kashan inapaswa kuvuka mipaka ya kikanda na kuwa na mchango katika kiwango cha kitaifa
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akiendelea kueleza viwango mbalimbali vya shughuli za Hawza, alisema: “Ikiwa tutataka kuzichunguza Hawza kwa kuzingatia upana wa maeneo yanayoathiriwa na aina ya majukumu yake, tunaweza kuzigawa katika viwango kadhaa.
“Baadhi ya Hawza hushughulikia zaidi mahitaji ya kielimu, kidini na kiutamaduni ya maeneo yanayozizunguka. Kundi jingine, pamoja na kujibu mahitaji ya eneo lao, lina uwezo pia wa kujibu mahitaji ya maeneo mengine na kuwa na ushawishi unaovuka mipaka ya kijiografia ya eneo husika.”
Ayatullah Arafi aliendelea kusema: “Katika kiwango cha juu zaidi, baadhi ya Hawza katika vipindi fulani vya historia hufikia nafasi ya kuwa na ushawishi katika kiwango cha kitaifa na katika mfumo mpana wa Hawza. Hawza za aina hii zinaweza kuwa vituo vya kuzalisha fikra, kuwalea wanazuoni na kutoa majibu kwa masuala mapana yanayoikabili jamii.”
Akisisitiza kuwa Hawza ya Kashan ina uwezo wa kufikia nafasi hiyo, alisema: “Tunachotarajia kutoka kwa wakurugenzi na viongozi wa Hawza ya Kashan ni kwamba waifikishe Hawza hii katika nafasi ambayo itakuwa na mchango katika kiwango cha kitaifa na hata zaidi ya hapo. Iwe ni Hawza ambayo, pamoja na kujibu mahitaji ya eneo lake, itakuwa na mchango wenye ufanisi katika kuwalea wanazuoni mashuhuri, kuzalisha elimu na kujibu mahitaji ya kifikra na kimaarifa ya jamii.”
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia historia ya kielimu na uwepo wa watu mashuhuri wa Hawza huko Kashan, alisema kuwa eneo hilo katika vipindi mbalimbali vya historia limewalea wanazuoni na wanafikra wakubwa. Watu ambao walikuwa na nafasi za juu katika elimu na maarifa, na ambao kazi na fikra zao zimeacha alama za kudumu katika historia ya elimu za Kiislamu.
Akizungumzia nafasi ya kielimu ya familia ya Naraqi na wanazuoni wengine wakubwa wa eneo hilo, aliongeza: “Kuwepo watu mashuhuri wa aina hii kunaonyesha kwamba Kashan ina uwezo mkubwa wa kielimu, kiutamaduni na vipaji vya thamani vya kibinadamu. Urithi huu wa kihistoria unapaswa kutambuliwa, kutambulishwa na kuhuishwa kwa njia sahihi.”
Ayatullah Arafi, akiwaelekeza Mkuu wa Wilaya, viongozi, wanazuoni na wakurugenzi wa Hawza ya Kashan, alisema: “Ni jukumu lenu kuibua na kuutambua uwezo huu wa kihistoria, kisha kuweka mipango ya kuutambulisha kwa jamii, hususan kwa kizazi kipya. Vipaji vya kielimu na vya Hawza katika eneo hili vinapaswa kutambuliwa na mazingira ya kuviendeleza na kuviwezesha kustawi yanapaswa kuandaliwa.”
Kuwalea wanazuoni wenye viwango vya juu, kuimarisha tafiti na kujibu mahitaji ya jamii
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akieleza matarajio yake kuhusu uongozi mpya wa Hawza ya Kashan, alisema: “Hawza tunayoipanga kwa ajili ya mustakabali inapaswa kuwa Hawza imara, inayoongoza, yenye kina cha kielimu na inayojengwa juu ya misingi halisi ya jadi ya Hawza. Inapaswa kuwa Hawza ambayo, sambamba na kuhifadhi urithi wa kielimu na kiroho wa zamani, pia ina uwezo wa kujibu mahitaji mbalimbali ya jamii ya leo ambayo yanabadilika kila mara.
“Hawza inapaswa kuwa hai katika nyanja za kuwalea wanazuoni mashuhuri, kuimarisha tafiti za kina, kuendeleza taaluma maalumu na kutatua changamoto za jamii. Pia inapaswa kuwa na uwezo wa kutekeleza jukumu lenye ufanisi sambamba na taasisi nyingine za kielimu na kiutamaduni.”
Ayatullah Arafi, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza shughuli za utafiti, alibainisha:
“Ni lazima kuimarisha mazingira ya utafiti, usomaji, ubunifu na uzalishaji wa maarifa katika Hawza. Hawza yenye uwezo wa watafiti na vipaji vya kielimu haipaswi kujitosheleza kwa mafunzo ya kawaida na yenye mipaka tu, bali inapaswa kushiriki kwa dhati pia katika nyanja mpya za kielimu na masuala yanayojitokeza hivi karibuni.”
Akizungumzia baadhi ya hatua na mabadiliko yaliyofanyika katika mfumo wa elimu na utafiti wa Hawza, alisema: “Katika kipindi cha hivi karibuni, mipango na miradi mbalimbali ya kuleta mageuzi na kuinua shughuli za kielimu za Hawza imeandaliwa, na sehemu ya mipango hiyo kwa sasa iko katika hatua ya utekelezaji.
“Kwa sasa, taaluma na mikondo mbalimbali ya kitaalamu inatekelezwa katika takribani mikoa 20 ya nchi. Mipango hii imeandaliwa kwa kuzingatia fikra za Imam Khomeini (r.a), matakwa ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na mahitaji ya jamii na dunia ya leo.”
Aliendelea kusema kuwa kuendeleza taaluma maalumu na kuimarisha mafunzo yanayoendana na mahitaji ya sasa ni miongoni mwa hatua zinazoweza kusaidia kuinua kiwango cha kielimu cha Hawza. Hata hivyo, juhudi hizo zinapaswa kuambatana na kuhifadhi misingi halisi ya jadi ya Hawza na kuimarisha misingi ya kielimu na ijtihadi.
Ayatullah Arafi, akizungumzia umuhimu wa ushirikiano kati ya Hawza na vyuo vikuu, alisema: “Tunashukuru kwamba vyuo vikuu nchini vimefikia nafasi nzuri za kielimu katika baadhi ya nyanja. Hawza nazo zinapaswa kutekeleza majukumu yake kwa namna inayolingana na wajibu wake, katika maeneo ambayo yanahitaji uwepo wake na kutoa majibu.”
Alifafanua: “Ushirikiano wa kielimu na kifikra kati ya Hawza na vyuo vikuu unapaswa kuimarishwa. Hawza zinapaswa kutumia uwezo wake wa kielimu, kiutafiti na kitaalamu ili kushiriki katika kutatua matatizo na kujibu maswali mapya ya jamii.”
Kuzalisha kazi za kitaalamu katika Fiqhi za kisasa na kuingiza Hawza katika nyanja mpya
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia baadhi ya mafanikio ya kiutafiti ya Hawza, alisema: “Katika miaka ya hivi karibuni, kazi na tafiti zenye thamani zimezalishwa na kuchapishwa katika mada mbalimbali za Fiqhi na masuala mapya yanayojitokeza. Mkusanyiko wa baadhi ya tafiti hizi umewekwa katika mfumo wa makumi ya juzuu za vitabu na kuwasilishwa kwa jamii ya kielimu.”
Akizungumzia kuongezeka kwa tafiti za Fiqhi katika nyanja maalumu, aliongeza: “Masuala kama Fiqhi ya tiba na nyanja nyingine za kitaalamu yanahitaji tafiti za kina na za kiijtihadi. Hawza zinapaswa kutumia uwezo wa walimu na watafiti mashuhuri katika kuzalisha maarifa na kutoa majibu yenye hoja madhubuti katika nyanja hizi.”
Ayatullah Arafi pia, akizungumzia suala la Akili Bandia (Artificial Intelligence), alisema: “Akili Bandia ni miongoni mwa masuala mapya ambayo yanaathiri nyanja mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Kwa sababu hiyo, inapaswa kuchunguzwa kwa mtazamo wa Fiqhi, sheria, maadili na maarifa.”
Aliongeza kuwa katika uwanja huu pia, kazi mbalimbali zimezalishwa katika Hawza, na mkusanyiko wa tafiti maalumu umewekwa katika mfumo wa juzuu kadhaa za vitabu na kupatikana kwa wasomaji.
Hatua hizi zinaonyesha kwamba Hawza inaweza, huku ikihifadhi misingi yake ya ijtihadi, kuingia katika masuala mapya yanayojitokeza na kujibu mahitaji mapya ya jamii.
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran alisisitiza: “Hawza ya Kashan nayo inapaswa kuelekea katika njia hii kwa kuzingatia uwezo wake wa kihistoria na kielimu, na kuandaa mazingira ya walimu, watafiti na wanafunzi wa Hawza wenye vipaji kushiriki katika nyanja mbalimbali za kielimu.”
Muqawama wa taifa la Iran ni jambo la kipekee katika mizania ya kimataifa
Ayatullah Arafi, akizungumzia hali nyeti ya kikanda na kimataifa pamoja na nafasi ya taifa la Iran katika mabadiliko ya hivi karibuni, alisema: “Taifa la Iran na Mapinduzi ya Kiislamu kwa sasa vipo katika mojawapo ya vipindi muhimu vya kihistoria vinavyoamua hatima ya taifa. Kulielewa kwa usahihi suala la hali ya sasa, kufahamu mabadiliko ya dunia na kutambua kwa kina nyanja mbalimbali za Muqawama wa taifa la Iran ni mambo yenye umuhimu mkubwa sana.”
Akisisitiza umuhimu wa kuzingatia nyanja mbalimbali za Muqawama wa taifa la Iran katika vita vya hivi karibuni, alisema: “Nimesema mara nyingi kwamba Muqawama wa mwaka mmoja wa hivi karibuni wa taifa la Iran ni jambo la kipekee katika medani ya kimataifa, na ili kuelewa nyanja zake mbalimbali, ni lazima kuzingatia athari na matokeo yake ya kihistoria na kisiasa.”
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akilinganisha harakati hiyo na baadhi ya vipindi muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, aliongeza: “Kama ambavyo ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 22 Bahman 1357 Hijria Shamsia (11 Februari 1979) uliathiri mizania ya kisiasa na kijamii duniani na kuonyesha nguvu mpya katika nyanja za kimaarifa na kisiasa, vivyo hivyo Muqawama wa taifa la Iran katika kipindi hiki nao umekuwa na athari na matokeo makubwa katika kiwango cha kimataifa.”
Aliendelea kusema: “Katika miongo iliyopita, taifa la Iran limepitia vipindi vingi vya kupanda na kushuka. Hata hivyo, kile kilichooneshwa katika Muqawama wa hivi karibuni kina sifa za kipekee kwa kuzingatia upana wa ushiriki wa wananchi, ushawishi wa kisiasa na mwitikio wake katika medani ya kimataifa.”
Ayatullah Arafi, akizungumzia mwitikio wa kimataifa kuhusu Muqawama wa taifa la Iran, alisema: “Katika kipindi hiki, kwa upande mmoja tumeshuhudia kuongezeka chuki, uhasama na uadui wa kambi ya ubeberu, hususan Marekani, dhidi ya taifa la Iran. Kwa upande mwingine, kumekuwa na mapokezi makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu na msimamo wa taifa la Iran miongoni mwa wananchi wa kawaida, wasomi na watu mashuhuri katika nchi mbalimbali duniani.”
Aliongeza: “Katika mikutano na mazungumzo niliyofanya na baadhi ya watu mashuhuri na viongozi wa nchi za nje, mwitikio wa Muqawama wa taifa la Iran na mtazamo wao kuhusu hali ya nchi yetu umekuwa miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa. Baadhi ya watu hao, wakizungumzia kiwango cha ufuatiliaji na uchambuzi unaofanywa kuhusu Iran katika mikutano na majukwaa mbalimbali, wamezungumzia nafasi na ushawishi wa Muqawama huu.
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran alibainisha: “Ukweli huu unaonyesha kwamba taifa la Iran, katika mazingira ambayo halikuwa na uungwaji mkono mkubwa na wa wazi kutoka kwa madola ya kigeni, limeweza kusimama imara dhidi ya shinikizo na vitisho kwa kutegemea imani, dhamira, mshikamano na uwezo wake wa ndani.”
Umuhimu wa kuhifadhi mshikamano wa kitaifa na kuimarisha Mhimili wa Muqawama
Ayatullah Arafi, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi umoja na mshikamano wa kitaifa, alisema: “Taifa, viongozi na taasisi mbalimbali za nchi wanapaswa kuzitambua kwa usahihi nyanja mbalimbali za uzoefu huu mkubwa. Mshikamano na ushirikiano wa wananchi katika kipindi cha vita ni mtaji wenye thamani kubwa ambao unapaswa kuhifadhiwa na kuimarishwa hata katika mazingira ya sasa, kwa kuzingatia hali na mahitaji yaliyopo.”
Aliongeza: “Leo pia, kwa ajili ya kuendeleza njia ya Muqawama na kulinda mafanikio ya nchi, tunahitaji moyo uleule wa kuhurumiana, umoja, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi wenye uelewa. Sehemu zote za nchi, kuanzia viongozi na wawakilishi hadi taasisi mbalimbali na wananchi wote, zinapaswa kujisikia kuwa zinawajibika katika njia hii.”
Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, akizungumzia ushiriki wa wananchi wa Kashan katika matukio mbalimbali ya kuiunga mkono nchi na Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: “Tulipokea taarifa kuhusu ushiriki na ushirikiano endelevu wa wananchi wa eneo hili katika kipindi chote cha matukio na vita vya hivi karibuni, jambo ambalo linastahili kupongezwa.
Wananchi wa Kashan, tangu siku za mwanzo kabisa, wamekuwa wakishiriki katika nyanja mbalimbali na kwa moyo wao wa kimapinduzi na kidini wamekuwa wakiunga mkono nchi na mfumo wa Kiislamu.
Mwisho, Ayatullah Arafi alimuomba Mwenyezi Mungu awajaalie wananchi wa Iran heshima na ushindi, akisema: “Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliimarishe taifa kubwa la Iran katika njia ya haki na Muqawama, azidi kuinua heshima na afya njema ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na makamanda wa kijeshi wa nchi, na atujalie sote mafanikio katika njia ya kupata radhi Zake, kutafuta radhi za Mtukufu Imam wa Zama (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), kuendeleza nchi na kuinua hadhi ya Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.”
Maoni yako